26 Oktoba 2022 - 17:54
Iran: Vikwazo kwa wazalishaji gesi kuwa na matokeo hasi

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuwa, hatua ya Wamagharibi ya kuziwekea vikwazo nchi zinazozalisha na kuuza nje ya nchi gesi itakuwa na matokeo hasi yasiyoweza kurekebishika.

Javad Owji alisema hayo jana Jumanne katika Mkutano wa 24 wa Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Gesi kwa Wingi Duniani (GECF), unaofanyika Cairo, mji mkuu wa Misri.

Owji ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo tayari kuisaidia dunia kuondokana na mgogoro wa nishati na kuhakikisha kuwa jamii ya kimataifa inakuwa na usalama wa nishati duniani.

Amebainisha kuwa, kutumia vikwazo kama wenzo wa kisiasa na kuzishinikiza nchi zinazozalisha kwa wingi gesi duniani kutakuwa na matokeo mabaya kwa mazingira, na kuzuia kufikia malengo ya maendelevu endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Mafuta wa Iran ameongeza kwa kusema: Katika muktadha huu, kuwekewa vikwazo vya upande mmoja au pande kadhaa mwanachama wa jukwaa hili (GECF), kwa mtazamo wetu, ni hatua ya kisiasa inayokinzana na kanuni na viwango vya sheria za kimataifa, na dhidi ya mantiki ya uchumi.

Javad Owji ameuambia Mkutano wa 24 wa Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Gesi kwa Wingi Duniani (GECF) jiji Cairo kuwa, uhaba wa gesi duniani umeziumiza nchi mbalimbali duniani, sanjari na kuyumbisha chumi za Ulaya, wakati huu ambapo nchi za bara hilo zinasumbuliwa na mgogoro wa nishati uliotokana na nchi za Magharibi kuiwekea vikwazo Russia.

Waziri Owji ameongeza kuwa, hata kabla ya vita vya Ukraine, Iran na Venezuela ambazo ni wazalishaji wakubwa wa mafuta na gesi duniani zilikuwa zimewekea vikwazo shadidi na Marekani.

342/